NITAWEZAJE KUMJUA MUNGU VIZURI ZAIDI
NITAWEZAJE KUMJUA MUNGU VIZURI ZAIDI
Shauku ya kila Mkristo ni kumjua Mungu vizuri. Kumjua Mungu vizuri kuna faida nyingi sana katika maisha ya mwamini, na kutomjua Mungu kuna hasara nyingi sana katika maisha ya mwamini.
Ukimjua Mungu vizuri, moyo wako utakuwa na amani kabisa (Ayubu 22:21). Kwa maana kumjua Mungu huleta imani na tumaini katika mioyo yetu. Mioyo ya waamini wengi imejaa hatia, hofu, wasiwasi, woga, kwa sababu ya kutokumjua Mungu vizuri. Kama tukimjua Mungu vizuri tutakuwa na amani tele.
Shetani amekuwa akitumia mwanya huo kusema na waamini maneno ya kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa katika imani, kwa maana anafahamu kabisa kwamba hatumjui Mungu vizuri.
Kumjua Mungu vizuri kutakusaidia sana hata katika maisha yako ya maombi. Kwa maana, utaomba sawasawa na mapenzi yake, kwa Mungu unayemfahamu vizuri (1 Yohana 5:14). Wakristo wengi wanaomba vibaya na hawapati kile wanachokiomba kwa sababu hawamfahamu Mungu vizuri, na wala hawajui kanuni za kupata kile wanachokiomba kwa kuwa hawamjui Mungu vizuri.
Kwa hiyo shauku yako iwe katika kumjua Mungu wako vizuri.
SWALI: Nitawezaje kumjua Mungu wangu vizuri?
Tunamjua Mungu vizuri kwa kulisoma neno lake kila siku kwa uongozi wa Roho Mtakatifu.
Unapokuwa unasoma neno la Mungu kila siku. Hapo ndio mwanzo wa kuanza kumjua Mungu vizuri zaidi na kwa ukaribu zaidi. Kwa maana Mungu hujifunua kupitia neno lake.
Unaposoma neno, utamjua kuwa Mungu ni Mungu wa upendo, ni Mungu mwenye rehema nyingi, ni Mungu anayesamehe, ni Mungu anayeponya, ni Mungu anayejibu maombi n.k
Huwezi kuyajua haya kama husomi neno lake.
Kwa hiyo kuanzia leo, wewe ambaye moyo wako unashauku ya kumjua Mungu wako vizuri na unashauku ya kuwa karibu naye. Anza kusoma Biblia yako kila siku.
MAOMBI:
"Ee Bwana Yesu, nina kiu na shauku ya kukujua wewe Mungu wangu zaidi. Ninaomba neema ya kulisoma neno lako kila siku katika jina la Yesu Kristo. Amina."
